Istilahi za Ushairi

Yafuatayo ni maneno ambayo mshairi au mwanafunzi wa fani ya ushairi atayapata mara kwa mara. Ni vema kuyaelewa na kuyajua kwa kina kwa sababu pasipo na hizi istilahi, hapana ushairi kamili.

1. Shairi

Shairi ni tungo yenye muundo na lugha ya kisanii na unaofuata utaratibu wa vina na mizani, hisi au tukio juu ya maisha au jambo na hufuata utaratibu maalum wa urari na muwala unaozingatia kanuni za utunzi wa mashairi yanayohusika.

2. Vina

Vina ni silabi za kati na mwisho wa mshororo au tenzi. Kwa mfano, katika ubeti ufuatao, vina vya kati ni ka ilhali vya mwisho ni ki.

Jambo litatatulika, iwapo halibaniki,
Halikosi bainika, faraja au la dhiki,
Lazima litasomeka, iwapo halisemeki,
Panapo moto hufuka, ishara hazifichiki.

3. Mizani

Mizani ni idadi ya silabi katika mshororo wa shairi. Kwa mfano, mshororo ufuatao una mizani kumi na sita:

Mo-la ndi-ye hu-tu-li-nda, i-na-po-ku-wa tu-hu-ma

4. Mshororo

Mshororo ni mstari mmoja wa maneno katika shairi. Idadi ya mishororo kwa kila ubeti wa shairi huainisha aina tofauti za mashairi. Kwa mfano, Tathlitha ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti. Ubeti ufuatao una mishororo mitatu.

Hata usake humwoni, hodari kwa yake kazi,
Hukusanya ya makani, yawe yake maongezi,
Udaku uso kifani, kwao wanayo ajizi.

5. Ubeti

Ubeti ni kifungu cha maneno katika shairi ambacho kimepangwa kwa mishororo kadhaa. Kwa mfano, shairi lifuatalo lina beti tatu.

Mawazo yananiwasha, ukweli nisielewe,
Yale unayonipasha, kwengine ukawa siwe,
Mawenge unaonesha, mwafulani usifiwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

Moto unaukokesha, patulivu pako wewe,
Unapenda kutonesha, kikajikita kiwewe,
Kigeugeu wazusha, yako tusiyatambuwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

Tumaini limekwisha, kuaminiwa si wewe,
Twajua wanaotosha, lijulikanalo liwe,
Yote unayotupasha, lazima yatatuliwe,
Kama popo unatisha, vilivyo tusikujuwe.

6. Istilahi nyinginezo

Muwala – ni mtiririko na mpangilio wa fikra kutoka ubeti hadi ubeti zinavyopokezana kwa kufuatiliza kisa au tukio katika shairi. Muwala hupima ufundi wa mtunzi kulingana na alivyoyapanga mawazo yake.

Utoshelezi – ni hali ya kila mshororo na kila ubeti kuwa na maana kamili. Maneno ya mshororo mmoja wa shairi yanapaswa kueleweka bila kutegemea yale ya mistari mingine.

Nathari – ni lugha ya riwaya ambayo si ya kishairi bali ni maelezo tu. Lugha yenyewe hutumia bila kutumia mpangilio au ufundi wowote wa kishairi.

Urari – ni mpangilio na ulingano wa mizani, mistari ya ubeti na usawa wa vina. Vina huwiana kiufundi bila kulazimisha maneno.

Uhakiki/Tahakiki/Uhariri/Tahariri – ni uchambuzi wa maandishi yoyote, vitabu au majarida kwa kufafanua kwa kina tathmini yake kwa kukosoa na kusahihisha. Hili hufanyika kwa kudadisi mbinu zilizotumika, maudhui, lugha na ufasaha, ukweli na uwongo uliomo ndani ya maandishi. Maoni hutolewa baada ya kufanya uhakiki.

Vipande – ni sehemu za mshororo ilivyogawanywa kwa alama ya kituo (,). Kila kipande kina jina lake kama inavyoelezewa hapa chini.

Ukwapi – kipande cha kwanza katika mshororo.

Utao – kipande cha pili katika mshororo

Mwandamo – Kipande cha tatu katika mshororo

Ukingo – kipande cha nne katika mshororo

Mwanzo/Kifunguo/Fatahi – mshororo wa kwanza katika ubeti

Mloto – mshororo wa pili katika ubeti unaofuata mwanzo.

Mleo – mshororo wa tatu katika ubeti unaofuata mloto

Kimalizio/Kiishio – mshororo wa mwisho katika ubeti usiorudiwarudiwa katika kila ubeti.

Kibwagizo/Kiitikio – mshororo wa mwisho katika ubeti unaorudiwarudiwa kila ubeti.