Mgogoro wa Ushairi

Kulingana na historia ya Ushairi, ni shahiri kuwa vikundi viwili vilizua mjadala mkali kuhusu maaana ya ushairi. Wanamapinduzi walisitiza kuwa mashairi ya arudhi yalimfunga sana mshairi kupasha ujumbe wake vizuri. Walidai kuwa mshairi hakuweza kujieleza vizuri kwa kuwa ilikuwa ni lazima ajibiidishe kwanza kutafuta maneno yatakayolinganisha vina na kutosheleza mizani. Waliamini kuwa mtunzi ana uhuru wa kutunga aina za mashairi wazipendazo bora tu wapashe ujumbe kwa hadhira. Washairi hao walitunga mashairi bila kujali arudhi za ushairi.

Tazama baadhi ya kauli za Wanamapokeo ambao waliamini Ushairi ni arudhi

SHABAAN ROBERT

“Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa sanaa ya vina, una ufasaha wa maneno machache au muhtasari. Mwauliza wimbo, shairi na tenzi ni nini? Wimbo ni shairi ndogo, ushairi ni wimbo mkubwa na utenzi ni upeo wa ushairi. Mwauliza tena kina na ufasaha huweza kuwa nini? Kina ni mlingano wa sauti za herufi. Kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti na ufasaha ni uzuri wa lugha. Mawazo na maoni na fikra za ndani zinapoelezwa kwa muhtasari wa shairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu”.

MATHIAS MNYAPALA

“Ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale. Ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa mizani na vina maalumu kwa shairi.” 1

ABDILATIF ABDALLA

“Utungo ambao katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja baada ya chenziye; wenye vipande vilivyo na ulinganifu wa mizani zisizo pungufu wala zilizo zaidi; na vipande hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalum na yenye lugha nyofu, tamu na laini, lugha ambayo ni tetelezi kwa ulimi kwa kuitamka, lugha ambayo ina uzito wa fikra, tamu kwa mdomo wa kuisema, tumbuizi kwa masikio ya kuisikia na yenye kuathiri moyo uliokusudiwa na kama ulivyokusudiwa.” 2

Tazama pia baadhi ya kauli za Wanamapinduzi

E KEZILAHABI

“Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno ya fasihi yenye mizani kwa kifupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha.” 3

M.M. MULOKOZI

“Ushairi ni mpangilio maalumu wa maneno fasaba yenye muwala, kwa lugha ya mkato, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au mawazo, kufunzaau kuelezajambo au hisi fulani kuhusu maisha ya binadamu kwa njia inayoburudisha na kugusa moyo.” 4

Marejeleo:
  1. Shaaban Robert, “Hotuba Juu ya Ushairi,” Journal of The East African Swahili Committee, 28/1 (1958)
  2. Mathias Mnyampala, Diwani ya Mnyampala, (Dar es Salaam Kampala/Nairobi: East African Literature Bureau, 1970); “Dibaji.”
  3. E. Kezilahabi, “Ushairi wa Mapokeo na Wakati Ujao,” katika kitabu cha J.P. Mbunda (Mhariri), Uandishi wa Tanzania: Insha, (Nairobi/Kampala/Dar es Salaam: East African Literature Bureau, 1975), uk. 23.
  4. M.M. Mulukozi, “Ushairi wa Kiswahili ni Nini?” Lugha Yetu, Na. 26 (1975), uk. 12