Usimdharau mwenzako. Jua hata yeye ni binadamu kama wewe. Ana haki kama zako. Mfanyie lile ungependa mwingine akufanyie. Binadamu wa Ukweli

Binadamu wa Ukweli

Kumbe wewe binadamu, mwenye miguu miwili,
Kumbe wewe una damu, isambaayo kwa mwili,
Kumbe wewe kama amu, binadamu wa ukweli,
Kumbe wewe sio chambo, binadamu wa ukweli.

Kumbe wewe sio chambo, cha kunifariji kweli,
Kumbe yako si ya kombo, una yako maadili,
Kumbe wewe sio chambo, kwa hicho kiwiliwili,
Kumbe wewe sio chambo, binadamu wa ukweli.

Kumbe hii ni kasumba, kukuona boromali,
Kumbe wewe sio kamba, kufungia haja kali,
Kumbe wewe sio pamba, timamu zako akili,
Kumbe wewe sio chambo, binadamu wa ukweli.

Kumbe una zako haki, unayo macho mawili,
Kumbe dhuluma hutaki, ingawa umehimili,
Kumbe umenihakiki, binadamu wa ukweli,
Kumbe wewe sio chambo, binadamu wa ukweli.

Kumbe nitakuhishimu, wewe u mja wa kweli,
Kumbe wewe u muhimu, mja wa mola halali,
Kumbe wewe una damu, timamu zako akili,
Kumbe wewe sio chambo, binadamu wa ukweli.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*