Shairi hili lilitungwa mwaka wa 2018 wakati elimu mfumo mpya ulianza. Je, mfumo wenye waendeleaje? Elimu Mfumo Mpya

Elimu Mfumo Mpya

Kwanza makubaliano, lisiwe jambo la baa,
Wafatilie mifano, tena liwe la ridhaa,
Wote waunge mkono, mfumo wakiandaa,
Kwa wote washika dau, liwe ni la manufaa.

Pili walipambanue, tofauti inafaa,
Wananchi watambue, lisiwe ni la fadhaa,
Tena wasilinyanyue, liwe la kutuhadaa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

Tatu walitekeleze, kila kona kuzagaa,
Vilivyo walieneze, tena kwa wake wakaa,
Pembeni walitembeze, ili kwa wote kung’aa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

Nne swifa walipambe, tusije tukakataa,
Sifa njema zikatambe, tisiseme ni balaa,
Nao weledi walumbe, bila domo kujikwaa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

Tano wasifuje mali, wala kadhongo kutwaa,
Wasiwanie fahali, bali fedha kuambaa,
Wasitende kama nduli, wakata wakisinyaa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

Sita wafuatilie, isiwe tu kutangaa,
Daima waangalie, hao wawe ndio taa,
Maovu wazuilie, lazima kama adaa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

Saba ninatamatia, ajili ya mtalaa,
Muda umeshawadia, ili mimi kunyamaa,
Si haba nimewambia, ili tuweze kupaa,
Liwe ni la manufaa, kwa wote washika dau.

© Kimani wa Mbogo (07/01/2018)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*