Usivunjike moyo kwa lolote linalokukabili. Wakati mwingine utavunjika moyo lakini hujui lijalo kesho. Leo utateseka lakini kesho huenda ukawa na heri njema. Heri Njema Iwe Kwako

Heri Njema Iwe Kwako

Sikiliza nakwambia, ewe bwana mdubiri,
Ulo karibu fifia, nisikize tafadhari,
Lile utalosikia, liige ulikithiri,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Wajiona na upweke, raha maishani huna,
Weye wajiona peke, sudi njema nayo huna,
hili wazo uepuke, tegemea Mola Bwana,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Mkata kinyongo hana, cha nini wajiwekea?
Bahati wasema huna, ukata wanyenyekea,
Hohehehe wajiona, bahati utapokea,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Ufukara wauona, na kujipuza kwa nini?
Kiatu wasema huna, cha kuvaa mguuni,
Mwengine mguu hana, yeye atasema nini?
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Unasema ni laana, mganga waenda kwake,
Warudi huku wanuna, ni kali shauri lake,
Mbuzi wa manjano huna, wa kumpeleka kwake,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Yohana kumi na nne, hapo sita Biblia,
Uisome kwa makine, Bwa Yesu ndiye njia,
Huu ugonjwa upone, jaribu kumtegemea,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Mwenyezi tunfuate,tuyatende yalo mema,
Nazo baraka tupate, kutoka kwake Karima,
Nakwambia yafuate, uupate usalama,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Siku moja itafika, mdubira bahatini,
Naye paka atasaka, panya nje pia ndani,
Yule paka kuteseka,naye bila bahatini,
Siku moja itakucha, heri njema iwe kwako.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*