Ni kuteseka, kufa na kufufuka kwake Yesu Kristo ambako kumewapa Wakristo ukombozi. Lisome shairi hili… Kifo Cha Yesu

Kifo Cha Yesu

Ushindi singeupata, na mshindi singekuwa,
Wokovu singeupata, mtu mwema singekuwa,
lakini nimeupata, na mshindi nimekuwa,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

Walimpiga Mwokozi, na mate kumtemea,
Katikati yao wezi, mabaya kumtendea,
Hawakuiona kazi, njema aliwatendea,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

Katikati yao wezi, Yesu alisulubiwa,
hawakujua Mwokozi, ukombozi wangepewa,
Leo njoo kwa Mwokozi, na wokovu utapewa,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

Walimdharau Bwana, wasijue ana jibu,
Wengine walimkana, lake jina kuharibu,
Ilikuwa na maana, alitwondolea tabu,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

Yesu Kristo alikufa, walipomtesa sana,
Walidhani nyingi sifa, zingeisha zake bwana,
Walidhani angekufa na sifa zake na jina,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

Ya tatu alifufuka, mbinguni akaingia,
Kifoni ameshatoka, cha enzi amekalia,
Karibuni atafika, njoo kwake kwake akwambia,
Kifo chake bwana Yesu, kimenipa ukombozi.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2007)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*