Lahaja za Kiswahili hutofautishwa kulingana na maeneo yake kama Kiunguja (kisiwani Zanzibar) ambacho kimekuwa msingi wa Kiswahili Sanifu, Kimvita (eneo la “Mvita” au Mombasa mjini, Kenya), ambacho zamani kilikuwa lahaja kubwa ya pili pamoja na Kiunguja, Kiamu (kisiwani Lamu, Kenya) na kadhalika. Lahaja Sineni


Lahaja Sineni

Mie kunena sineni, usingoje n`tanena,
Endapo niishi pwani, lahaja tamaa sina,
Heri nirudi barani, nitimize yangu dhana,
Kibanjuni siongei, kwetu ni mpeketoni.

Lugha yangu siharibu, vijineno siingizi,
Ya mama n`tajaribu, niikaliapo mbuzi,
Kusafiri merikabu, ya lahaja siongezi,
Kimvita siongei, kwetu ni Mpeketoni.

Nendapo Tanzania, ntaongea sanifu,
Huko Tanga kuingia, lugha yetu nisarifu,
Sinaye wa kumwambia, lugha yetu tusisifu,
Kimtangata sineni, kwetu ni Mpeketoni.

Pwani ya Tanzania, hata niende kusini,
Huko Kilwa kuingia, lahaja zao sineni,
Kutulia tatulia, niendapo ugenini,
Kimgao siongei,kwetu ni Mpeketoni.

Kongo nielekeapo, lahaja sitaipenda,
Langu la ukweli lipo, dhana yangu itashinda,
Kongo nishaingiapo, sitatoka kwa kibanda,
Kingwana sitaongea, kwetu ni Mpeketoni.

Huko Kongo nitatoka, nisafirie melini,
Unguja kupumzika, nirudi Mpeketoni,
Mashairi n`taandika, kuko huko visiwani,
Kitumbatu siongei, kwetu ni Mpeketoni.

Nende Pemba kisiwani, washairi niwapate,
Nijifunze kwa makini, nielekeapo Pate,
Lahaja mbovu sineni, niruhusiwe nipite,
Kipemba sitaongea, kwetu ni Mpeketoni.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*