Mambo yamebadilika. Si kama zama zile. Maadili, taadhima na tamaduni hazipo tena. Twaelekea wapi? Maadili Yamekosa


Maadili Yamekosa

Wa karibu na wa mbali, sana nimepeleleza,
Umezidi ujahili, mwanga umekuwa kiza,
Wazee hawahimili, machungu yawauguza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Ya heshima ni muhali, malimwengu yatatiza,
Yamekwisha ya awali, mila tulizotukuza,
Ya zama wamebadili, bora yaliyowongoza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Wamezidi wanawali, haya yao yashangaza,
Wanaudhi marijali, kwa maovu waigiza,
Taadhima ni dhalili, kwa kina nimechunguza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Huwapati wafadhili, wawao watakubeza,
La muhimu ndilo mali, ni kigezo cha kuweza,
Mkata huwi kamili, vijana watakutweza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Maneno ya pilipili, hawakosi kuchokoza,
Huzitoa chembe kali, yawapo ya kutangaza,
Wamezidi mafidhuli, hadhi yao kupunguza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Siku hizi hawajali, kwa maovu wajituza,
Hawaahidi la kweli, wakawa wanatimiza,
Mwongozo ni taamuli, tabia kuzieneza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

Waadimika halili, watendavyo na kuwaza,
Nimebaki kusaili, sinaye kunieleza,
Hakika sijakubali, mwema atajitokeza,
Yamekosa maadili, yatendwayo yachukiza.

© Kimani wa Mbogo (14/05/2013)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*