Kwenye uga naingiya, adimu kuwaarifu,
Sijaja kuwachukiya, wala yeyote kusifu,
Ya maisha kuwambiya, kwa njia ya ufanifu,
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
Yalo mengi ya duniya, adhimu na usumbufu,
Yaja mema kwa mabaya, ya ushujaa na hofu,
Japo twaimba hodiya,twabakia wakosefu,
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
Siku nyingine twakoya, Mwenye Enzi twamsifu,
Siku njema twaingiya, tunao uchangamfu,
Hakunaye wa kuliya, twajivunia unyofu,
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
Hata ije tutagaya, hakuna mlaanifu,
Neema itatujiya, tufikapo kuwa jifu,
Mengi atatutendeya, mwenye upole Latifu,
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
Hatupaswi shika taya, wala kuwa na uchofu,
Katu tusije kupaya, zaja baraka sufufu,
Pamwe tufurahi ghaya, yajapo ya ufanifu
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
Nanga sasa natiya, yangu nimewaarifu,
Naishika yangu njiya, nimelonga yangu kifu,
Siyapendi ya hekaya, siyaambi ya urefu,
Maisha safari ndefu, maji kujaa na kupwa!
© Kimani wa Mbogo (31/05/2008)