Mapenzi huwa hiari. Hufai kulazimishwa kupenda. Iwapo utalazimishwa, haki zako zahujumiwa. Litazame shairi hili lililotungwa kwa ushirikiano wao Kimani wa Mbogo na Muna Moons Ahmed. Mapenzi Huwa Hiari

Mapenzi Huwa Hiari

Kimani wa Mbogo:

Upendo huwa saburi, huamki ukatenda,
Mapenzi yaliyo heri, hayafanyiki kwa inda,
Mahaba hufanywa siri, hadharani hutoshinda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Upendo usio shari, kwa upana unawanda,
Mapenzi yanashamiri, nyoyoni yanapotanda,
Mahaba yanojihiri, kukua hayatodinda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Upendo unoamiri, kwa wawili huwa nyonda,
Mapenzi si utajiri, kwa mapeni yatarunda,
Mahaba yanapojiri, pasiwe wa kuwalinda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Upendo ni wake mwari, kipata nayempenda,
Mapenzi huja kuhiri, wawili wakiyaunda,
Mahaba huwa habari, hadharani kutoranda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Upendo ni umahiri, unapendwa na makinda,
Mapenzi ni ikirari, ukakubali kupenda,
Mahaba yao vigori, vilelenihuwapanda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Upendo si wa ayari, ujanja hutokufunda,
Mapenzi yatahitari, ya satua ukatenda,
Mahaba si kughairi, ukaamua kuenda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda!

Muna Moons Ahmed

Mapenzi si kuajiri, kumlipiza alopenda,
Mapenzi hutusitiri, alo mkubwa na kinda,
Mapenzi ukiabiri, utavishwa hata sanda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi kweli khatari, usipovuna matunda,
Mapenzi mfano pori, tatafuta wa kuwinda,
Mapenzi kama bahari, mawinguni yakitanda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi kishayakiri, ujifunge kwa ukanda,
Mapenzi yatahadhari, kinawiri tu kwa bunda,
Mapenzi kishawa nari, mishipayatakuganda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi si uhodari, waezapaa na kudunda,
Mapenzi si ushairi, matamuunavyopinda,
Mapenzi yataka ari, utavuna ulopanda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi ilo kiburi, katu huwezi ilinda,
Mapenzi hayana shari, kikinaiutakonda,
Mapenzija misumari, mbao itapigwa randa,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi kimpa daktari, ‘taugua kwa kitanda,
Mapenzi humuathiri, akauguzakidonda,
Mapenzi yakishajiri, pete ulivishe chanda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

Mapenzi takuwa shwari, ikibarikiwa nyonda.
Mapenzi kiwa tayari, tafika unakoenda,
Mapenzi tajivinjari, waja wakuone mwenda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwikupenda.

Mapenzi kiwa shubiri,umeharibu ajenda,
Mapenzi huwa safari, kitimia utapenda,
Mapenzi ni ya Qahari, kijalia utashinda,
Mapenzi huwa hiari, hulazimishwi kupenda.

© Kimani wa Mbogo (08/10/2010)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*