Huu hapa waadhi wa mzazi kwa mwanawe. Waadhi Wa Mzazi (Ngonjera)


Waadhi Wa Mzazi (Ngonjera)

MWANA:
Babangu ninalo swali, kwa kweli lanisakama,
Jicho unalo fahali, sitakwambia tazama,
Swali langu la fasili, hatupati hali njema,
Nieleze nielezwe, mbona tukose baraka?

Mkata hapendi mwana, pendo nimeona lako,
Zamani baraka mboka, mlikuwa mwapatako,
Kwa siku hizi hakuna, naliona badiliko,
Nieleze nieleze, Mbona baraka sioni?

BABA:
Mwanangu na unipate, utege lako sikio,
Wana siku hizi wote, waadhi huwa pambio,
Wanaloambiwa lote, hawategi masikio,
Mwanangu tega sikio, na waadhi ufuate.

Ili upate baraka, kwa wazazi fanya vyema,
Hali njema ukitaka, mwena uwe na heshima,
Wazazi, dada na kaka, kwao iwe taadhima,
Mwanangu tega sikio, na heshima iwe ada.

MWANA:
Hakika nimesikia, kuwa jaha nifuate,
Hili la kutangulia, kuwa heshima nipate,
Waadhi kuusikia, ili niweze kupita,
Nieleze nieleze,ninayo hamu kujua.

BABA:
Basi sikiza mwanangu, uufuate waadhi,
Vazi lako nalo tangu, naliona linaudhi,
Mwili wote wa mwanangu, na yeyote kumkidhi,
Mwanangu tega sikio, vazi liwe ni la jaha.

Ukivaa vazi lako, jisetiri mwili wote,
Ile teitei yako, urefu nayo ipate,
Liwe pana lote lako, hishima nawe upate,
Mwanangu tega sikio, uvae vazi la jaha.

MWANA:
Langu lisilo la jaha, lile nitatekeleza,
Nataka niwe shabaha, inavyopendeza nyiza,
Yote haya mrahaba, wala sio ya kutweza,
Nieleze nieleze, ili niwe mwana mwema.

BABA:
Ya taifa lugha yetu, enyi nyote mwabadili,
Nayo nyingine tukutu, ile ya ubaradhuli,
Ile ninyi mwadhubutu, kudharau Kiswahili,
Mwanangu tega sikio, lugha yako yaniudhi.

Mawasiliano yote, yawe ya kueleweka,
Uendapo pale pote, lugha yetu kuitaka,
Hii ienezwe kote, ili iwe yatukuka,
Mwanangu tega sikio, haya yote ufuate.

MWANA:
Babangu nashukuru,yangu yote kuungama,
Hayo yote niwe huru, niweze kuyaandama,
Maishangu naamuru, kuyatenda yalo mema,
Nieleze nieleze, kila siku unionye.

Na sheshe niwe daima, kwa yote kutadhibiri,
Niwe mwenye kutazama, lolote linalojiri,
Shukrani kwa Karima, naomba unipe heri,
Nieleze nieleze, kila siku unionye.

© Kimani wa Mbogo (01/01/2008)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*