Bonface Khaemba Wafula

Uandishi ni kipaji adimu na kama vile kipaji chochote kile huhitaji kupaliliwa na kuchochewa mara kwa mara. Uandishi huchochewa kwa kusoma zaidi na kufanya utafiti zaidi. Ili uzidi kubobea katika uandishi, mazoezi ni kitu muhimu sana. Huwezi kuwa mwandishi kama huandiki, mshairi kama hutungi au mwalimu kama hufundishi. Uandishi ni tunu adhimu na adimu yenye uwezo wa kuibadili jamii kwani hutumika kama kioo cha kuitazamisha na kuibadili jamii. Mwandishi katu halali; atasifu, atakashifu, atafariji, ataburudisha na kuielimisha jamii. Bila waandishi jamii iko kwenye giza totoro.

MAISHA YAAWALI
Bonface Khaemba Wafula alizaliwa mnamo mwaka wa 1987, katika kijiji cha Musamba, eneo bunge la Matungu katika kaunti ya Kakamega akiwa kifungua mimba katika familia ya Bwana Ernest Wafula na Bi Tina Wafula. Mnamo mwaka wa 1994 alijiunga na shule ya msingi ya Khalaba nilikosomea hadi alipofanya mtihani wa darasa la nane mnamo mwaka wa 2001.

Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Namamba mnamo mwaka wa 2002 alikosomea hadi alipohitimu cheti cha kuhitimu masomo ya shule ya upili( K.C.S.E) mnamo mwaka wa 2005. Akiwa shule ya upili hasa kupitia kwa ushauri wa mwalimu wake wa Kiswahili marehemu Vincent Lumbasi ari na hamu ya kujua vipengele kadhaa vya lugha ya Kiswahili ilizidi kukua ndani yake na kumfanya asome na kuandika zaidi hasa mashairi ya Kiswahili. Baada ya kukamilisha masomo ya shule ya upili, Bonface alijiunga na Chuo Cha Walimu cha Shanzu Mombasa  alikosomea kati ya 2007 na 2009 na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Cha Masinde Muliro, Kakamega kujiendeleza kitaaluma.

UANDISHI
Kipaji cha uandishi kilichipuka akiwa bado shule ya msingi punde tu alipofahamu kusoma na kuandika. Insha zake zilikuwa zikitumiwa na mwalimu darasani kama nyenzo ya kuwafundisha wanafunzi wengine namna ya kuandika insha bora. Akumbuka nikiwa darasa la sita mwalimu wake wa Kiswahili Bwana Mathias Wawire akimtabiria kuwa aidha atakuwa mwandishi au mwanahabari.

Ubunifu wake wa visa vya kusisimua na umaizi wa lugha sanifu ya Kiswahili ulikuwa wa kupigiwa mfano. Hoja zake nzitonzito katika mijadala shuleni ilichangia pakubwa katika kumutia moyo kuwa alikuwa na kipaji kilichohitaji kupaliliwa. Alipojiunga na shule ya
upili ya Namamba mnamo mwaka wa 2002 katika kidato cha kwanza, aliteuliwa kama mwenyekiti wa chama cha waandishi chipukizi shuleni. Jukumu lake kuu lilikuwa ni kufuatilia matukio shuleni, nchini na hata nje ya nchi na kuwapasha wanafunzi wenzake gwarideni kila ijumaa na jumatatu. Nyakati za michezo ya shule za upili, alikuwa akiandamana na timu ya shule yao kwenda kuandika ripoti za michezo na kuzisoma gwarideni shuleni. Alipofika kidato cha pili, aligundua alikuwa kipaji cha utunzi wa mashairi hasa baada ya kumtungia shairi mwalimu wake wa Kiswahili bwana Vincent Lumbasi (ambaye sasa ni marehemu)  akimtakia shufaa ya haraka baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani. Pia Boniface alianza kuandika michezo mifupi mifupi ambayo waliigiza katika siku za wazazi shuleni.

Mnamo mwaka wa 2012 akiwa mwalimu wa Kiswahili katika shule ya upili ya Namamba alitunukiwa jukumu la kutayarisha, kuhariri na kusimamia uchapishaji wa jarida la shule, kazi ambayo aliifanya kwa ufundi wa hali ya juu.

Mnamo mwaka wa 2017 alianza kuyatuma mashairi yake kuchapishwa kwenye gazeti la Taifa Leo na Taifa Jumapili katika ukumbi wa Ushairi wenu na ukumbi wa Sokomoko. Kwa kuongezea ameandika mswada wa ushairi ambao uko kwenye hatua za uhariri. Mswada huu ukishachapishwa utakuwa kama taa ya kuwaongoza wanafunzi wanapokabiliana na maswali ya ushairi. Mswada huu unahusu istilahi mbalimbali za ushairi, namna ya kujibu maswali ya ushairi, mifano ya maswali na majibu ya ushairi na zaidi ya mashairi thelathini yenye miundo,maumbo na maudhui mbalimbali. Kando na kazi za ushairi, pia ameandika hadithi fupi mbalimbali ambazo ananuia kuziorodhesha kwenye diwani moja majaliwa. Baadhi ya hadithi fupi ambazo ameandika ni pamoja na hadithi ya zamu yea ambayo ni tashtiti ya viongozi wanaochukulia nafasi za uongozi kama upenyu wa kunyakua na kujilimbikizia mali ya umma.

Kando na utunzi wa mashairi na uandishi wa hadithi fupi, Bonface ana mpango wa kutia guu kwenye uandishi wa riwaya na tamthilia pamoja na hadithi za watoto.

Naazimia kuandika na kuchapisha zaidi ya vitabu ishirini katika aushi yangu vitakavyosomwa kote nchini na hata nje ya mipaka ya Kenya. Nachochewa mno na kazi za waandishi mahiri wa humu nchini kama vile, Profesa Ken Walibora, Daktari Wamitila, Ustadh Wallah bin Wallah, Daktari Timothy Arege, Bi Pauline Kea na wengineo.

UALIMU
Bonface alianzia kazi ya ualimu katika shule ya upili ya Namamba mnamo mwaka wa 2010 punde tu baada ya kukamilisha mafunzo ya ualimu katika chuo cha walimu cha Shanzu. Uweledi na umilisi wake wa somo la Kiswahili ulimwezesha kuimarisha matokeo ya wanafunzi katika somo hilo. Mnamo mwaka wa 2012 alitunukiwa cheti cha kuwa mwalimu bora zaidi katika kaunti ndogo ya Matungu baada ya kuwaongoza wanafunzi kupata alama ya wastani ya 9.796(B+) katika somo la kiswahili kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne. Rekodi hii bado haijavunjwa hadi wa leo shuleni na pia katika kaunti ndogo ya Matungu. Baada ya miaka mitano shuleni Namamba, alihamia mjini Nakuru na kujiunga na shule ya upili ya St. Monica Lanet mnamo mwaka wa 2015. Akiwa mwalimu katika shule ya St.Monica Lanet, aliweza kutambua na kukuza vipaji vya uandishi miongoni mwa wanafunzi wengi wakiwemo Francis Ameyo, Eddie Hassan, Edith Wambui na wengineo. Mnamo mwanzoni mwa mwaka wa 2018 alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Anestar Lanet ambapo angali hadi sasa kama mwalimu wa somo la Kiswahili na somo la Historia na pia mwalimu msimamizi wa chama cha waandishi cha Anestar(A.B.I) na mwasisi wa chama cha Kiswahili cha Anestar( CHAKIA).