Moses Chesire

Ushairi ni kipera kimoja cha fasihi ya Kiswahili,dhima ya ushairi sawa na fasihi ya Kiswahili ni kuonya kufunza kuelimisha n.k. hivyo basi washairi wanapozitunga kazi zao walenge kuielimisha jamii na kuifanya iwe bora zaidi. Kwa hivyo ushairi utumiwe kama kioo cha jamii.

Jina lake ni Moses Kipchirichir Chesire kutoka gatuzi la Trans-nzoia, wilaya ya Kwanza, katika kijiji cha Kapsitwet. Ni mwalimu wa shule ya msingi ya Kitubo iliyopo wilayani Kwanza na anatambulika kwa lakabu ya shairi kama Sumu ya Waridi.

Moses alianza masomo yake katika shule ya msingi ya Kodiaga katika gatuzi la Kisumu baadaye kuguria shule ya msingi ya Tandui katika gatuzi la Baringo alikomalizia masomo yake ya msingi. Alijiunga na shule ya upili ya Bartolimo iliyopo Baringo Kaskazini na baadaye kujiunga na Taasisi ya ualimu katika chuo cha walimu kusomea cheti cha Ualimu. Hatimaye alijiunga na chuo kikuu cha Egerton alikosomea shahada ya Elimu ya msingi akiegemea somo la Kiswahili.

Alianza kupenda ushairi akiwa katika shule ya msingi aliposhiriki katika mashindano ya kughani mashairi. Wahadhiri wake katika chuo kikuu walimfa sana kumwonesha ulimwengu wa washairi tajika kama Shaaban Robert, Mathias Mnyapala na Abdilatif Abdala.

Shairi langu la kwanza nililitunga nilipokuwa katika shule ya upili ya Bartolimo na kulitumia kuwaburudisha wageni waalikwa katika siku ya wazazi shuleni.

Mashairi yake huegemea sana masuala ibuka yanayokumba jamii, huangazia suala ambalo limemtendekea binafsi au katika jamii anamoishi au taifa. Shairi kama Kamari Kamaliza linawatahadharisha vijana dhidi ya madhara ya kamari na Luthuli tumepajua linalowahusia wananchi kuhusu matapeli waliojaa LuthulI. Huwa anachukua takribani nusu saa kutunga shairi lenye beti tano na muda huo hupungua iwapo shairi lina beti chache.

Mashairi yake yote huwa ya arudhi, huzingatia kanuni zote za utunzi wa mashairi ya kimapokeo, mashairi yanayostahiki sifa ni yale yenye kuzingatia arudhi, haya mengine yanayoandikwa kinathari, haoni kama ni ushairi wa kiswahili bali umefuata mtindo wa ushairi wa kizungu

Kutokana na kipawa cha utunzi wa ushairi na umilisi wa lugha, Moses ameweza kualikwa kuwa mfawidhi katika dhifa mbalimbali.

Ameweza kupata marafiki wengi mno kupitia kumbi za ushairi mitandaoni hususan Facebook na WhatsApp.

Moses anapania kuandika diwani yake katika siku zijazo. Vilevile anatarajia kutumia mtandao kuupanua uwanda wa ushairi.

Moses anasema kuwa wapo watu mtandaoni wanaowavunja moyo washairi wakisema watu wa bara hawaijui lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, hawawezi kutunga mashairi ya Kiswahili.

Kwa sasa, Moses ni mwalimu wa shule ya msingi, vile vile huwa refa wa kambumbu na huishabikia Arsenali.