Mwanagenzi aliye na ari na bidii katika masomo yake, hakosi kufaulu. Mwanagenzi Mtafiti


Mwanagenzi Mtafiti

Naja tena na ripoti, niwapashe ukumbini,
La ukweli siwafiti, naliandika tungoni,
Ninakupisha uketi, utafakari makini,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Mwachuoni hapiti, kwa mwendo wake chuoni,
Hata angapiga goti, amwombe Mola Manani,
Kileleni hajipati, kutoenda vitabuni,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Kusoma sana hasiti, ana ari mshindani,
Anaposoma haoti, ama ende vitandani,
Utukutu haufati, kutwa yu makitabani,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Vijiani humkuti, kizurura mitaani,
Hapendi ya ati ati, kusemasema hanani,
Kutwa ana chake kiti, habishani hagombani,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Ashindane hajinati, asemalo si utani,
Hajitii katikati, liso lake halumbani,
Hupenda somo kwa dhati, afuzu taalumani,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Kujilinda yu thabiti, wangamtisha vitani,
Mishale huidhibiti, ingerushwamatusini,
Mzalendo hasaliti, hana udhia chuoni,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

Usumbufu hauleti, amani iwe chuoni,
Liso lake halifati, lazima ombe idhini,
Hukupigia suluti, kwa taadhima si duni,
Mwanagenzi Mtafiti, hufaulu hatimani!

© Kimani wa Mbogo (30/08/2010)

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*