Mama

Lukuki zangu natuma, salamu kuwafikia,
Kisha nianze nudhuma ujumbe kuwaambia,
Kuwahusu kina mama, sie walojizalia.
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Mama mama tena mama, mara tatu narudia,
Tumtunzeni kwa wema, ni mengi alopitia,
Ishi ukimtazama, sache kumtumikia,
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Majukumu lijituma, wewe akakwangalia,
Kuhakiki u salama, huna shida wapitia,
Akawa wako uzima, dawama afurahia,
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Tangu hujui kusema, hadi sasa waongea,
Dede hadi hivi wima, watembea wakimbia,
Kukukimu hakukoma, kwacha kukuhudumia,
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Hebu kumbuka ya zama, vuta zako nadharia,
Wakati hayupo kama, ukawa wamlilia,
Leo una taadhima, mbona wamtupilia?
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Usambe wamsukuma, akakosa kuridhia,
Laana takuandama, kila utapopitia,
Utabaki kulalama, ufukara kukungia,
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Kitaka njema karama, na amani ya Jalia,
Basi yako mama, anachokihitajia,
Baraka nyingi neema, hapo zitakushukia,
Umlipe kipi mama, hadhi aloshikilia?

Nishawasili hatima, hapa nanga naitia,
Hakikisha yako mama, nia amekusafia,
Ninayo mpe heshima, na wengine kufatia,
Umlipe nini mama, hadhi aloshikili?

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *