Anionee Mbawazi

Ninakutuma kipungu, uende kwa laazizi,
Kisha wende wanguwangu, uruke bila henezi,
I dhalili hali yangu, umwambie sijiwezi,
Anionee mbawazi.

Haya ruka tumwi wangu, tarishi wangu nyerezi,
Zipaze habari zangu, paa kama umpazi,
Arudi tucheze gungu, tuzaze chetu kizazi,
Anionee mbawazi.

Nampenda toka tangu, sijapenda wala juzi,
Mweleze nna utungu, mueleze wazizi,
Kwamba kupumua kwangu, ni heri tu ya Mwenyezi,
Anionee mbawazi.

Yaniwanga rasi yangu, utokepi usingizi?
Mawazo yenye mizungu, kuchwa ndio yangu kazi,
Mwambe mahabubu wangu, siupati usingizi.
Anionee mbawazi.

Yeye yu sindano kwangu, na kwake mie ni uzi,
Libasi yu kanzu yangu, namremba ni darizi,
Ni rabana mwenziwangu, bila iye langu vazi,
Anionee mbawazi.

Macho naona ukungu, yamepofuka maozi,
Hata visikizi vyangu, sisikii masikizi,
Mwambie huyo dadangu, kutwa nina bumbuazi,
Anionee mbawazi.

La matozi kubwa wingu, limetanda la matozi,
Nimekiri kosa langu, nishajua ni mpuzi,
Natubu kwake na Mungu, tena siyarudilizi,
Anionee mbawazi.

Arudi kipenzi changu, tuwe halua kwa lozi,
Nimeshanunua changu, anipikie mtuzi,
Nile hadi tani yangu, Changu kwa wali wa nazi,
Anionee mbawazi.

Hebu atazame mbingu, ye mwenyewe hajulizi!
Imewangia tewengu, si ng’ombe wala si mbuzi,
Nimetubu muhibangu, Anionee mbawazi,
Anionee mbawazi.

Kwangu sio bangubangu, tu kama mwili na ngozi,
Utalii na mzungu, kwa kuwa ananijazi,
Yu mwiba ni nungunungu, silaha yangu azizi,
Anionee mbawazi.

Mboni sinitie pingu, ndiye yangu maolezi,
Mbona anipiga rungu, nimekonda kama uzi?
Asisikize majungu, kunikosesha gonezi,
Anionee mbawazi.

Ni ashara beti zangu, na thineni tamatizi,
Naumwa na wangu wengu, hubani kupiga mbizi,
Huba li vikwazo chungu, si si si ja sisimizi,
Anionee mbawazi.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *