Mbona Wakutie Dhiki

Haambiwi mwenye ozi, katu haambiwi ola,
Haamshwi usingizi, haamshwi liyelala,
Na malaji haulizi, mwenye ndaa ya chakula,
Mbona wakutie dhiki?

Mbona ukampe ngozi, msasi msaka swala,
Au mbawazi kwa kozi, kumuonesha kitala?
Nawe mwenza hujulizi, vi sawa lila na fila?
Mbona vikutie dhiki?

Hazidishi hapunguzi, kwa mema wala madhila,
Hapunguzi haongezi, majinuni majuhula,
Mja awapo mpuzi, huwa ni jaa jalala,
Mbona likutie dhiki?

Muuzi na mnunuzi, japo tatizo ni hela,
Harufu na manukizi, waridi sio langila,
Hukupunguza mashuzi, mnyima kunde kuzila,
Mbona akutie dhiki?

Si sawa mbwa na mbuzi, tarishi si seremala,
Mja mwenye maonezi, si kipofu asoola,
Hadumu katu bazazi, adumupi kabaila?
Mbona akutie dhiki?

Alo nayo masikizi, ni heri amesikila,
Haya yangu magombezi, kituo nawatilila,
Tundua kwa tunduizi, utaona ya fadhila,
Hivyo sikutie dhiki.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *