Waharibifu Mwambongwa

Kwenu nyie wapanguzi, wapangua yalopangwa,
Ja njuga yenu mavazi, kwa waja kuleta nongwa,
Panyofu hupakombozi, ikapeta midolongwa,
Waharibifu mambongwa.

Mvua inyapo nyerezi, hupaomba pawe jangwa,
Umoya kwenu tukizi, mnaohibu kutengwa,
Wadumizi wadukizi, msiotaka kupingwa,
Waharibifu mambongwa.

Walivyo kama mikizi, wakiruka huborongwa,
Japo hawana mapezi, u nswi kwao hutungwa,
Wakazipiga na mbizi, nchi kavu wakazongwa.
Waharibifu mambongwa.

Kutakata hawawezi, si wang’avu wangasingwa,
Wazuri uchinjigizi, kwa kujiona mabingwa,
Hebu wambie utwezi, kutwa kucha wakigangwa,
Waharibifu mambongwa.

Hamsa ndo zangu hizi, beti tamu kama chungwa,
Chengo changu makaazi, ni mkaazi wa Gongwa,
Kimia changu cha juzi, yalikuwa yanachangwa,
Waharibifu mambongwa.

© Rashid Mwaguni Mgute.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *