Vyawaje? 

Nimeyachunguza sana, nikaona yashangaza,
Ndipo kwamba nikanena, wajuao kunijuza,
Ningali jawabu sina, ni sibabu ninauza,
Vyawaje kwa adinasi, kutoona sikiole?

Kwa hayawani aina, hili jambo wanaweza,
Masikizi kuyaona, ni jambo walifanyiza,
Sijabaini maana, kutwa kucha ninawaza,
Vyawaje kwa adinasi, kutoona sikiole?

Si jambo kutaniana, kwa kebeha mkabeza,
Ni tata tangu ni mwana, waleo lanitatiza,
Mbona hulioni mbona, sikiolo kusikiza?
Vyawaje kwa adinasi, kutoona sikiole?

Ni la tangu si la jana, suala ninouliza,
Nawaza tena na tena, leo hini natangaza,
Nilijue lake shina, la asasi na mwangaza,
Vyawaje kwa adinasi, kutuona sikiole?

Mwenzenu ni mwenye mwina, lindi la mwina wa chiza,
Nawachia waungwana, swalangu kunijibiza,
Buriani buriana, jibuni mnaoweza,
Vyawaje kwa adinasi, kutoona sikiole?

© Rashid Mwaguni.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *