Shubiri Tamu

Harufuyo ni ya mvuje, kwangu mimi ni haramu,
Uliponamba ningoje, mie mbio timu timu,
Nipende pendo liweje, ungali kwangu u sumu,
Ikafana hutendwaje, shubili ikawa tamu?

Pindipo unipembeje, nikuone muadhamu,
Nikukurubie nije, uwe wangu mhashamu,
Siji hata ufanyeje, ni heri unilaumu,
Ikafana hutendwaje, shubili ikawa tamu?

Hubalo tunda la jaje, ngozi yake nje ngumu,
Basi umelaniwaje, nisile nikashutumu,
Liache huba livuje, imefika yako zamu,
Ikafana hutendwaje, shubili ikawa tamu?

Na huko kwako nijeje, nawe ulinidhulumu,
Yakini jina si mboje, Radhia huna nidhamu,
Amba hata uambeje, siji nijepata pumu,
Ikafani hutendwaje, shubili ikawa tamu?

Eti”fanya hala uje, kumbe nawe una hamu,
Mali yangu uyafuje, uyakamue ja ndimu,
Kwa mtawi nirudije, mja usonikirimu,
Ikafana hutendaje, shubili ikawa tamu?

©Rashid Mgute Mwaguni.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *