Ulimwengu 

Huu ulimwengu pofu, hauni uoendako,
Mezua tele uchafu, hao waishio huko,
Uchafu wa kilihafu, misiba na susuiko,
Hauoni uendako, huu ulimwengu pofu.

Haombwi tena raufu, kila uchao vituku,
Kondo nyingi zimeshufu, zikaleta sokomoko,
Ukengeushi ndo safu, ikatupwa mbali miko,
Huu ulimwengu pofu, hauoni uendako.

Ni karata na turufu, utabaka gawanyiko,
Kukazuka masharifu, walo na hadhi na mbeko,
Kazi ya mja hafifu, ikawa kijungu jiko,
Hauoni uendako, huu ulimwengu pofu.

Na wingi ubadhirifu, kula hadi kiso chako,
Israfu israfu, ikatwaa miondoko,
Ikawa uharibifu, dhuluma na lalamiko,
Huu ulimwengu pofu, hauoni uendako.

Nyamatinde na nyamafu, vikapikwa kwenye jiko,
Uovu na taklifu, vikenda kuima koko,
Uko wapi uongofu? hakuna tena hauko,
Hauoni uendako, huu ulimwengu pofu.

Wa katiba uvunjifu, kila mtaa wendako,
Haramu kama ni sufu, ikafanywa kwenye soko,
Vitenda vilaanifu, ukabeba ubeleko,
Huu ulimwengu pofu, hauoni uendako.

Waja wenye majisifu, wakajiita viboko,
Lengo i wapi sarafu? inatafutwa iliko,
Ndipo maovu sufufu, yakajaa fokofoko,
Hauoni uendako, huu ulimwengu pofu.

Beti nane kamilifu, nakoma zangu nyandiko,
Mauja ni mapotofu, tuyafanyie maziko,
Tuzue mazoefu, tulilete badiliko,
Huu ulimwengu pofu, hauoni uendako.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *