Mbuga Zetu Tuzitunze

Ujumbe naunudhumu, usambae nchi nzima.
Kutukuza umuhimu, mbuga zetu za wanyama.
Wameleta mwetu humu, watalii darahima.
Dawama tuzitukuze , mbuga zetu za wanyama.

Kila msasi haramu, tumripoti mapema,
Kwani yeye ni dhalimu, kwa kuutenda unyama.
Mbuga anazihujumu, uchumi unadidima.
Dawama tuzitukuze, mbuga zetu za wanyama.

Hupendeza kwa utamu, hayawani kutazama.
Kisha twapata ilimu, wanyama tukiwasoma.
Tutunze mbuga zidumu, tuzizuru kila juma.
Dawama tuzitukuze, mbuga zetu za wanyama.

Tungane sote kaumu, mbuga tuzitunze vyema.
Na hasa yatulazimu, tuzuru bila kukoma.
Wenyeji tushike zamu, na wageni wawe nyuma.
Dawama tuzitukuze ,mbuga zetu zawanyama.

Mpunguti kule Lamu, na Tsavo tuna Mzima.
Wanyama twawafahamu,asadi ngwena na duma.
Tutazamapo kwa hamu, hufurahika mitima.
Dawama tuzitukuze, mbuga zetu za wanyama.

Ukingoni nishatimu, nawaaga kaditama.
Kwa beti sita tamimu, nakoma yangu hatima.
Sasa ni yenu awamu, utunzaji kujituma.
Dawama tuzitukuze, mbuga zetu za wanyama.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *