Si Kazi Kudamirika

Wimapo paangalie, unaweza kuanguka,
Ulimwengu uujue, dawama hubadilika,
Kila kilele alie, na chini pia hushuka,
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wa juu pia hushuka.

Sikiliza nikwambie, kwinamako huinuka,
Nako kulojinukie, huja kukateremka,
Bahari iangalie, hupwa na ikajazika,
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wa juu pia hushuka.

Beuo simfanyie, mwenzio akadunika,
Kejeli umchezee, kwa tadi kwenda jivika,
Pale ulopakalie, naye anaweza fika,
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wajuu pia hushuka.

Dunia mviringie, ni tiara yazunguka,
Hata kiza kiingie, hucha kukapambazuka,
Mwenza usimuumbue, mipango ni ya Rabuka.
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wa juu pia hushuka.

Wenza tusijichekee, kwa kuwa kwetu yanyoka,
Ijapo tujipangie, tuliyo sie twataka,
Huenda ayapangue, Rabbi mpa na mpoka,
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wa juu pia hushuka.

Ukingo niahirie, Mola mwenye mamlaka,
Duati tujiombee, kwa zake nyingi baraka,
Sini tusijigambie, na wenza tukawacheka,
Pavumapo palilie, si kazi kudamirika,
Wa juu pia hushuka.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *