Pendo

Pendo lina ncha mbili, farahani na udhia,
Ni shubili na asali, ladhaye nnakwambia,
Kiliambata madhali, sichoke kuvumilia,
Loo!Moyo na hisia, vitatakapo suguana,

Hakunaye wala nguli, gwiji alolishindia,
Kutoka hapo azali, dahari ya zamania,
Yakini lina thakili, hufanya mtu kulia,
Loo!Tamuli na moyo, vikija shirikiana,

Mtima na taamuli, likija kuviingia,
Siha hujawa dhalili, kwa mawazo kuwazia,
Hasa asipokujalo, ulo msafia nia, Loo!
Mwawazo na moyo, vikija kuzidiana,

Mahaba ni nyongo kali, ya ngwena yaigizia,
Si rahisi ni shughuli, nalo kwandamana ndia,
Utaweza kuhimili, vishindo vikikujia? Loo!
Moyo na zitendo, vitakapokutendana.

Kwa haya yangu kalili, mapenzi kwenye dunia,
Kiduchu sana ya kweli, kitaka kujipatia,
Tahadhari tafadhali, usije kujijutia, Loo!
Moyo na ilani, hasa kwa sie vijana.

© Rashid Mwaguni

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *