Nakupenda Penzi Moto

Kitandani mejilaza, hino kweli ndoto yangu,
Kwa hamumu nakuwaza, njoo ubavuni mwangu,
Waraka wako sikiza, mepinda mtima wangu,
Mahadhiyo yaniliza, na upweke zidi kwangu,
Wewe kweli ndiye wangu.

Kifuacho natamani,  kukigusa sitosita,
Wewe kwangu ni mwandani, taitika kiniita,
Kumbuka haya ya usoni, myaka kumi ikipita,
Utakuwa wa thamani, na rembeo metameta.
Kipepeo nakupenda.

Figa lako ndilo tosha, lavuruga yangu akili,
Najiona nimekwisha, kukupenda nina kibali,
Na huzuni kuitorosha, kwa fahari kunikubali,
Nimepandwa na motisha, ya kupata wako mwili,
Kukuwaza ninakonda.

Swali lako liuliza, kawa nini penzi mwisho,
Hivi sasa nakujuza, ni bahari iso mwisho,
Ni kwa mungu ‘sisitiza, Adamu Hawa wanzisho,
Penzi tamu naagiza, kama asali ndo lisho.
Raha huzua karaha.

Nijuacho na karaha, ni donda lisotibika,
Taishia na kuhaha, na vizazi taabika,
Kwa sasa sio mzaha, tuwe macho na mipaka,
Tuishie kwa furaha, na wanja nitakupaka,
Tuepuke na wambeya.

Ni milima hikutani, wanadamu hupatana,
Usiali na ni lini, kwa umbali metubana,
Ngozi yako ni laini, sautiyo ya kufana,
Sitakutupa jamani, ombi langu kufaana,
Uwe wangu wa milele.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *