Swali Hino Zushi

Wawaza ukijichosha, na haya ya ulimwengu,
Swali lako lapotosha, ni kufuru kwa mungu,
Kustaajabu maisha, ni kujitia machungu,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

Atanguliapo kuku, basi yai huliega,
Yai likipona buku,huagua kifaranga,
Kutaga kuku sio chuku, hakuhitaji mkunga,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

Ya dini kitafakari, kaumba vyote jalali,
Wanasanzi mekiri, dunia kisulisuli,
Mambo mengi ni ya siri, hayahitaji maswali,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

Kuku ni yai twajua, si shinde kujikanganya,
Yai ni kuku elewa, wacha kutabaranganya,
Ya dini kuingiliwa, laana wazu kusanya,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

Mwanzo wetu ni Adamu, tamati yetu kiama,
Wewe mjinga ka sanamu, hujui za kale zama,
Swali lako li dhalimu, na akilizo zi nyuma,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

Ni upuzu lako swali, kelelezo mesikika,
Nakusihi we rijali, kule shamba wewe fika,
Jitafutie sahali, hilo jembe wewe shika,
Cha kwanza kutangulia, ndicho chanzo cha kingine.

© Brian Mutambo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *