Twajenga Twabomoa

Uwanjani naingia, mtimani nachomeka
Madhila mwashuhudia,  magazeti memulika
Wanakenya twaumia , kuchapo twanungunika
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

Baragumu pulizia, wabakaji wamefurika
Binti metuharibia, ubikira mewatoka
Ndwele mewalimbikizia, kovu kawazunguka
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

Raslimali bugia, jamani mtatosheka?
Ndi ndi mmeshikilia, mwahofia kungatuka
Ufisadi mesalia, daima wasikika
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

Nasakamwa na udhia, damu inanikauka
Wahaka wanivamia, matozi nibubujika
Umoja umefifia, utu mesahaulika
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

Maadili kizingatia, uhasimu tutazika
Vilio vitatulia, uchumi taimarika
Upendo kinyunyuzia, Kenya mpya tajengeka
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

Tamatini nimefika, zingatia nilomulika
Mwenyezi kijalia , barakaze zitashuka
Maishani tatulia, nyoyo zitaridhika
Uzalendo dumisheni, liendeleze taifa

 © Nyangara Mayieka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *