Atakupenda Ulivyo?

Hata Mola kakulinda, utawaza na kukonda,
Zurura kote enenda, simwoni kipofu kinda,
Macho yake amewanda, kuona unachotenda,
Atakupendaulivyo, asipende uli’navyo?

Akitizama kibanda, mara abekue gunda,
Simwoni asiyependa, aushi kuishi Runda,
Raha njema ya kuponda, si ya kesho kuikanda,
Atakupenda ulivyo, asipende uli’navyo?

Mishipa itamganda, kusema yako ajenda,
Nyota waiponda, masikitiko waunda,
Wamkataza kupenda, umtae akaenda,
Atakupenda ulivyo, asipende uli’navyo?

Ungalinunua tunda, huliachi lake ganda,
Kupiga la maji funda, kutomeza ndiyo inda,
Muhibu atakupenda, weye na yako mabunda,
Atakupenda ulivyo, asipende uli’navyo?

Wende mtini kutunda, hata majani yatanda,
Ungasema ni matunda, majani chini taenda,
Kupenda atakupenda, japo kwa unayotenda,
Atakupenda ulivyo, asipende uli’navyo?

© Kimani wa mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *