Nikubali Usuhuba

Beti hizi natungia, we mrembo sally vera,
Hakika mwanivutia, wang’ara kila mara,
Simu nikikupigia, usidhani nakukera,
Kidosho nakulilia, nikubali usuhuba.

Mja mosi kusalia, kutwa kucha kapera,
Mwandani kujitafutia, suluhisho la busara,
Sibadili yangu nia, kufuate kama dira,
Kidosho nakulilia, nikubali usuhuba.

Nashindwa kutulia, ni mapenzi mfukara,
Sitaki wa kudandia, ila aso na honera,
Sababu kuangukia, meleza pasi hasira,
Kidosho nakulilia, nikubali usuhuba.

Tamati nimefikia, elewa yangu dhamira,
Kando yangu karibia, upate yalo nadra,
Hakika hutajutia, mapenzi kukuzingira,
Kidosho nakulilia, nikubali usuhuba.

© Lawrence Gaya