Mwiba Mtungu

Ni sononi mtimani, jitimai nitawala
Metahayari usoni, ni masimango yanila
Ukaniwata dondani, mevurugika kulala
Mola sinipe mapenzi, wa kupendwa kadimika

Yakanitoa pangoni, hubani kasalitika
Kajifunga kiunoni, mahabani kavutika
Nikadhani wa ubani, kumbe ni kapu la taka
Mola sinipe mapenzi, wa kupenda kadimika

Mejitia mashomboni, lujani ukanizika
‘Kanitia hamasani, uchao nabobojoka
Majuto maishani, mbasi kanigeuka
Mola sinipe mapenzi, wa kupenda kadimika

‘Linitosa utumwani, kaniteka katekeka
Ja kopo msalani, kanitema kama taka
‘Liyemdhani mwendani, adui kageuka,
Mola sinipe mapenzi, wa kupendwa kadimika

‘Mezama mrututuni, ndani ninaungulika
Kupenda sitamani, uwehu menizuzuka
Kakufuta akilini, ni lini yatafufuka?
Mola sinipe mapenzi, wa kupendwa kadimika

© Nyangara Mayieka

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *