Huwi mswahili kwa kuzaliwa uswahilini. Tabia tu ndizo zitafanana lakini asili yako itabaki. Lisome shairi hili… Katu Huwi Mswahili


Katu Huwi Mswahili

Hujitapii usuli, kudhani hatubaini,
Tangu zama sikubali, hata utunge ughani,
Usitufanze dhalili, ukitubwagia zani,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Arudhi sana twajali, kwendeleza hino fani,
Za kunongesha kauli, hizo kwetu hazifani,
Wajivunia kalili, tungo tunazothamini,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Twaelewa majabali, vigogo hawajivuni,
Wajuao huwa tuli, hawasemi hadharani,
Si jambo la maadili, kujisifu kiamboni,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Tutakuona fidhuli, wa kuvuruga amani,
Tukukemee vikali, hata ukijiamini,
Mienendo yake nduli, himfai maishani,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Ingalipo mihimili, sakafu hadi darini,
Si ukuta kukabili, uzito wa paa uzani,
Si hoja kulala chali, ushike paa kononi,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Nimesema wazi hali, soma tena kwa makini,
Nimewarushia boli, kwenu huko uwanjani,
Fungeni sasa magoli, twawatazama wavuni,
Kuzawa Uswahilini, katu huwi Mswahili!

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*