Nakupenda Kama Dodo

Ewe banati Mulamba, ung’araye kama nyota,
U mweupe kama pamba, macho yako yanameta,
Umenifunga kwa kamba, penzi letu limenata,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Wewe kati ya adimu, ya vidosho duniani,
Kwangu naomba udumu, uwe wangu maishani,
Ukanipe tabasamu, daima nikuamini,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Ninajaza kama pipa, ewe wangu wa  ubani,
Mahaba unayonipa, yamekwama akilini,
Kukumwaga ninaapa, sitaweza asilani,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Nitazidi kukupenda, Naomi halua langu,
Mabaya sitokutenda, lo! yatakupa uchungu,
Mbali nami ukienda ‘tateseka hani yangu,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Umekuwa yangu shibe, ukafukuza upweke,
Natamani nikubebe, mgongoni nikuweke,
‘Kupeleke Entebe, tunywe chai kwa matoke,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Wewe u wangu ubavu, ulonipa usingizi,
Kanifanya mnyamavu, nikiwa kwenye malazi,
Ukaumbika shupavu, ikawa muruwa kazi,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

Nakupenda sana rembo, ndo maana nakusifu,
Katikati ya warembo, u namba moja kwa safu,
Wang’ara bila mapambo, karembeka maradufu,
Banati Mulamba wangu, nakupenda kama dodo.

© Lawrence Gaya