Mnameza Mate

UPINZANI:

Serikali sikiliza, tuna jambo la kuamba,
Lolote tutawapaza, ukweli tutauimba,
Jukumu kutekeleza, mmekuwa mwisho namba,
Ufisadi mmekuza, uchumi wayumbayumba,
Zi wapi zenu ruwaza? ahadi zagonga mwamba.

SERIKALI:

E Upinzani tazama, kisiki jichoni lote,
Kabla kutuandama, kiondoe kisiote,
Mnapenda kulalama, utulivu tusipate,
Hatamuni tutakwama, miongo miwili yote,
Leo tunakula nyama,  nyinyi mnameza mate.

UPINZANI:

Ndiyo mnakula nyama, hino nyama ya kadhongo,
Uvivuni mmezama, kwa ahadi za uongo,
Kwa Hatamu moja nzima, hatujui lenu lengo,
Enda nyumbani mapema, achia wenye mipango,
Zi wapi zenu ruwaza? Ahadi zagonga mwamba.

SERIKALI:

Mmekuwa debe tupu, kelele kupiga sana,
Mu watu gani taipu? Maendeleo kukana,
Mtoboe hino jipu, lisiwasumbue tena,
Pia kaza yenu zipu, washindani muwe bwana,
Leo tunakula nyama, nyinyi mnameza mate.

UPINZANI:

Kusema haijalishi, kutenda ndo kufuata,
Vi wapi ‘pakatalishi? Mlosema mtaleta,
Hatarini tunaishi, alshababu twateta,
Msione tu wabishi, amani hatujapata,
Zi wapi zenu ruwaza? Ahadi zagonga mwamba.

SERIKALI:

Hata akilia chura, ng’ombe atayanywa maji,
Tunaongoza kwa kura, sijifanye wajuaji,
Hamjui nani bora, rais muwaniaji,
Na mwasema kila mara, mtatua hili taji,
Leo tunakula nyama, nyinyi mnameza mate.

© Lawrence Gaya