Mambo huja na kupita, kwa mtu mwenye imani,
Mambo mazito na vita, mengi huja maishani,
Ila nguvu tumepata, tuelewe kwa makini,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.
Ni furaha kubwa sana, kusoma mengi ya Mungu,
Furaha hiyo yafana, ikijua sana Mungu,
Huwa jambo la maana, Kumtegemea Mungu,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.
Furaha tunda la roho, someni Wagalatia,
Zawadi toka kwa roho, Mungu ametupatia,
Yapo mengine ya roho, tena moyo yanatia,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.
Furahini siku zote, ombeni bila kukoma,
Shukuru kwa mambo yote, ukitumaini mema,
Mungu muweza ya yote, huyo ndiye wa rehema,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.
Wakati wote furahi, hata uwapo kwa dhiki,
Rafiki ninakusihi, furaha kwako ibaki,
Awapo nawe Masihi, milele huaibiki,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.
La furaha hutakosa, Mungu unapomwamini,
Huizuia mikasa, na kutupa tumaini,
Hupati nguvu kwa pesa, watu wanazotamani,
Ipo furaha ya Bwana, ambayo ni nguvu yetu.