Karaha ya Kamari

Kwa machozi naandika, mfuko umetoboka,
Akiba nilizoweka, leo zimeshatoweka,
Pesa nimefilisika, nimebaki kuteseka,
Kamari uliniteka!

Kamari uliniteka, kanifanya mraibu,
Hela nyingi nilisaka, pasi bahati nasibu,
‘Nyonya’ nimekubandika, iwe ni yako lakabu,
Kamari nimeudhika!

Kamari nimeudhika, kisogo changu nakupa,
Nimepoteza dakika, na riziki hujanipa,
Kwako tena sitafika, gwenje zangu umetupa,
Kamari sijaridhika!

Kamari sijaridhika, senti nyingi kuchuma,
Huna la kutamanika, ufukara unafuma,
Waama nimesumbuka, ukwasi nikauhama,
Kwangu kasahaulika!

Kwangu kasahaulika, hatima nikifikia,
Mekoma kulalamika, sauti yangu sikia,
Nawe utahangaika, tamati wakaribia,
Siku yako itafika!

© Lawrence Gaya