Wapi Ulipo?

Zimepita nyingi siku,   toka kwako ‘jasikia,
Nakuwaza kila siku, nashindwa kuelezea,
Nimejaza langu buku, hisia kuelezea,
Wapi ulipo kimwana, nipate kukufikia

Usiku kucha silali, waniruka usingizi,
Siijui yako hali, u mzima laazizi?
Metamani kiukweli, nikuone laazizi,
Wapi ulipo kimwana, nipate kukufikia

Kiwa ndwele ulipata, nijuze nipate fika,
Shaka moyoni mepata, hakina mesononeka,
Ikiwa nitakupata, mtima utatulika,
Wapi ulipo kimwana, nipate kukufikia.

Moyo umeukatili, kwa hakika umepapa
Tokea wangu halili, moyo wangu kuuzipa
Umepasuka kikweli, rudi furaha kunipa
Wapi ulipo kimwana, nipate kukufikia

© Justine Orenge