Wanavyotunga siku hizi ni ajabu! Wanayaita mashairi ila hayakubaliki kuwa mashairi. Njooni washairi mnieleze! Mashairi Gani Haya?


Mashairi Gani Haya?

NYANGEMI ninalo swali, hizi tungo zinatisha,
MWAIbadilisha hali, Kingereza kuwatosha,
La uhuru mnafeli, mkitunga ya kupasha,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Twaa la kabila mbali, hatutaki kubaini,
Lugha yetu Kiswahili, toka Nyanza hadi Pwani,
Sanaa ndiyo twajali, hatutaki iwe duni,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Ninaona una mambo, mitihani gani tena?
Vipo vingi vya kimombo, vikundi vya kulumbana,
Ukishindwa ya mafumbo, kunyamaza kutafana,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Ama wende Wingereza, Kiswahili huthamini,
Mbinu ziko kutongoza, si jina langu kughani,
Hino lugha ukibeza, sinyamazi ukumbini,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Tumia kasha la Sheri, utuwache kwa amani,
Hilo litakuwa heri, si la kwetu hadharani,
La hapa ni mashairi, si ya Uzungu kubuni,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Tu hapa kufunzana, si vurumai kuzua,
Lisiwe kukinzana, wala lugha kuumbua,
Wawili kusemezana, si hapa kujifutua,
Ni sanaa gani hii, mashairi gani haya?

Ndio “magwiji” wa sasa, tena wajuao sana,
Wanaovizua visa, na la maana hawana,
Lao huwa ni siasa, tena wingi kujivuna,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Swila wanivunja mbavu, nikiihofia fani,
Napenda ukakamavu, kama wako ukumbini,
Tena huo welekevu, kwa haraka kubaini,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Hatua ichukuliwe, maji yamezidi unga,
Heri kitanzi atiwe, akioneshwa kutunga,
Hisani asitendewe, kanuni anazipinga,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Ubunifu si kukera, kutunga yasiyofana,
Mkiona tunagura, msisaili kwa kina,
Mjue twalinda sera, za fani kwa kila kona,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Hii kweli imekufa, si sanaa tulojuwa,
Ya kujizolea swifa, pasi na kujitambuwa,
Sitasubiri maafa, yaharibu nachojuwa,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Mwatupamba la aibu, hino fani kuumbua,
Watatucheka ajabu, hadhira ikitambua,
Yameshakuwa harabu, mashairi yaungua,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Ukitunga soma tena, urekebishe mizani,
La muhimu liwe vina, mada yako kuibuni,
Uichore yako dhana, yeleweke ukumbini,
Hii ni sanaa gani, mashairi gani haya?

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*