Nipe Ahadi Mpenzi

Nakutamani moyoni, kidosho nakulilia, 
Nakupenda siutani, hakika hunivutia, 
Dumu nami maishani, pamoya tukasalia, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Huba ongeza mvuto, yawe laini ja pamba, 
Kwetu yawe motomoto, yawake kama maramba, 
Tuwe sawa kwa mpito, tufungane kwayo kamba, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Niahidi kuyalinda, mahaba yetu wawili, 
Namba wani kunipenda, katu nisiwe wa pili, 
Hata milima kipanda, mapenzi yawe kamili, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Nifanye wako uhai, kila tyimu nipumue, 
Kuishi nami tumai, mie wako kupendae, 
Sio Machi si Julai, mahaba tupalilie, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Nami takupenda hani, sitokuacha milele, 
Takuzamisha hubani, tulivu bila kelele, 
Damuni na fuwadini, pate hanjamu belele, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Waseme menipa dumba, siti nitakuwa wako, 
Tujuane kwa vilemba, kwao vibaki vituko, 
Nitakuwa lako shamba, vuna huba sosumbuko, 
Nipe ahadi mpenzi, daima hutoniacha.

Nina mangi yakusema, ila penzi lanizidi, 
Kalamu yakwamakwama, damu yawaka shadidi, 
Yanibidi kutuama, kumipenda niahidi, Sauti Njiwa natua, moyo wangu wakupenda.

Mwalimu Mwangi,
Sauti ya Njiwa,
Naivasha, Kenya.