Mwanangu Ipo Siku

Maisha ni kujikaza, uvumilivu kuvaa
Naweze piya angaza, huhitaji kuduwaa
Japo mbale wazipwaza, na kuvua vidagaa
Mwana wangu ipo siku

Siku yaja kwa haraka, ewe mwana vumilia
Ufukara tatoweka, tijarani tazamia
Na tatago utavuka, tawa huru na huria
Mwana wangu ipo siku

Yatawa ni storia, hadithi kwa wajukuu
Yote liyoyapitia, safarini hadi juu
Uvivu litupilia, nawajue vitukuu
Mwana wangu ipo siku

Jitahidi kisabuni, baa zote zitapita
Kulalia guniani, katu tena hutajuta
Hutatweta shokoani, ulova utaupata
Mwana wangu ipo siku

Na libasi utavaa, mararu yawe stori
Matoni utawafaa, soni zako kisetiri
Utawa wa manufaa, kwa piya waso nakheri
Mwana wangu ipo siku

Nalo kasri utajenga, la kuvutiya matoni
Tayasahau majanga, yalokusinya moyoni
Hewa safi utapunga, matoni pa majirani
Mwana wangu ipo siku

Mwa Mwangi,
Sauti ya Njiwa,
Naivasha.