Kwaheri Kaka Wire

Kifo jijizi jahili, katuibia mndugu,
Kamficha kwa jabali,mpendwa kakangu,
Uwizi uso halali, wasababisha uchungu,
Kwaheri kakangu, ya munkari tupashe.

Kifo mchawi mkubwa, waroga hata mchana,
Ailetu mpendwa, hai kamtoa jana,
Katufanya kupatwa, na misongo ya vijana,
Kwaheri kakangu ya munkari tupashe.

Kifo ewe mfisadi, waadhibu mja nyofu,
Mekera yetu fuadi, kumfanya awe mfu,
Wadidi yetu idadi, tuna chuki kwa sufufu,
Kwaheri kakangu, ya munkari tupashe.

Kifo tatukoma lini? Afyetu kumaliza,
Wapenya pasi idhini, maishetu kutatiza,
Kwa Rabuka tuamini, huzuni tatamatiza,
Kwaheri kakangu, ya munkari tupashe.

© Lawrence Gaya