Niache Zako Uende

Kabla mangi unitende, nakuasa ukaende,
Kabla usazwe vipande, nafsiyo kwanza kalinde,
Nakuamba kajipende, unasutwa hivi punde,
Niache zako uende, uso fikra ewe mende.

Baradhuli huyu mende, jiasisi zote pande,
Haja gani ujipinde, ja kiwavi kwenye kunde?
Sijiko ikakupande, malimwengu yakukande?
Niache zako uende, uso fikra ewe mende.

Mbona bei usipande, unahongwa peremende!
Wajishasha unishinde, jitazame kila pande,
Japo mori zikupande, wewe bado duni mende,
Niache zako uende, uso fikra ewe mende.

Umetoka uniwinde, takulaza chali mende,
Kunyanyuka kukushinde, ndipo imani upende,
Wewe ni kama umande, litachomoza uende,
Niache zako uende, uso fikra ewe mende.

¬© Vitalis w’Esonga