Tuipande Miti

Tupande mbuni, tupate, kahawa kinywani,
Kwa mdalasini, tupate, kiungo mloni.

Mkaajabali, tupate, dawa ya machoni,
Kwa mshelisheli, tupate, tunda chemsheni.

Tupande mkanya, tupate, dawa mauani,
Na kwa mvungunya, tupate, mandhari mitini.

Tupande mtonga, tupate, matunda vinywani,
Kwa mkomamanga, tupate, kwendesha fungeni.

Tupande mng’ongo, tupate, dawa kifuani,
Kwa mkatafungo, tupate, kamba magomeni.

Tupande mtini, tupate, toka kwake tini,
Kwa mdoriani, tupate, zake doriani.

Tupande mbuyu, tupate, ladha chakulani,
Tupande mkuyu, tupate, diro aridhini.

Tupande mkwara, tupate, fimbo pia kuni,
Na kwa mkwakwara, tupate, mboga kwa majani.

Tupande mpesi, tupate, nguvu mishipani,
Mkoniferasi, tupate, kurasa mbaoni.

Panda mkamasi,, tupate, mlo telezini,
Na kwa mkakasi, tupate, urefu laini.

Kwa mkarafuu, tupate, kiungo mloni,
Kwa mkunatuu, tupate, dawa ya jandoni.

Panda mbingiri, tupate, kutapishiani,
Kwa msonobari, tupate, majano mbaoni.

Tupande mkoko, tupate, dawa ya ngozini,
Na kwa mtomoko, tupate, tomoko kondeni.

Tupande mkumbi, tupate, kili kupikeni,
Na kwa mbirimbi, tupate, ladha acharini.

Tupande mkaa, tupate, dawa kohozini,
Na kwa mkandaa, tupate, rangi kofiani.

Panda mtumbati, tupate, ugumu mbaoni,
Kwa msanapiti, tupate, nakishi uani.

Tupande mkoronge, tupate, ua mijengoni,
Tupande mkenge, tupate, vivuli mijini.

Panda mkunazi, tupate, kunazi vinywani,
Na kwa mbaazi, tupate, mbegu vitumboni.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *