Unapotoka Wamukota

Nilipopata habari, umeiramba rimbwata,
Nduguyo nikafikiri, ni majirani salata,
Lakini sasa nakiri, mwenyewe nimekupata,
Umelogwa wamukota, ama sitarehe zako.

Kisima waraukia, maenge ukitafuta,
Moto uje kuvuvia, kwa kuni ulotafuta,
Kutwa unang’ang’ania, uchafu kuutafuta,
Umelogwa wamukota, ama sitarehe zako.

Maswali najisaili, kuhusu jinsia yako,
Wewe ni mume kamili, ama gumegume huko,
Nakujuza unafeli, katika nikaha yako,
Umelogwa wamukota, ama sitarehe zako.

Nakuaga nikitoka, nazidi kushadidia,
Ukweli unapotoka, uzibadilishe tabia,
Kuna kazi kina kaka, kuzifanya ni hatia,
Umelogwa wamukota, ama sitarehe zako

© Moses Chesire