Jinamizi

Jana ndoto linijia, kote kumejaa damu
Sijui likotokea, tena yao binadamu
Mana nalisubiria, meuliza wanajimu
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Ngeu ilitapakaa, aridhini na maweni
Mito nayo ikajaa, ikamwaga baharini
Sijaona tena baa, ‘lohiliki taifani
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Insi walijifia, mabondeni na nyikani
Jasadi zikabakia, kuliwa na hayawani
Sijui yao hatia, lopeleka kuzimuni
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Tama nikajishikia, mafuvu ‘lipoyaona
Nika’nza kuriaria, moyo upate kupona
Tena nikapiga dua, nikimusihi rabana
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Nikaona wanijia, visu vikimeremeta
Toba nikajililia, nikinywea nikitweta
Macho akitumbua, nikajua kimepata
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Mara nikashitukia, kokoiko ya kikwara
Ndotoni sikujifia, wala mkuki kugwara
Lakini najiwazia, walikuwa makafara?
Waganga naulizia, kitale lama lamu

© Moses Chesire