Nakuaga Mpenzi

Nakuaga laazizi, yakimwaika machozi,
Hakika ninamaizi, weye rafiki azizi,
Hakuthamini feruzi, bila wewe sijiwezi,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Hiki kitu cha mapenzi, hasa ikiwa penziyo,
Hukufurahisha pumzi, ikuingiapo moyo,
Utamu wake wa danzi, ukiila pasi choyo,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Kwangu umekuwa kito, iliyo nyingi thamani,
Urafiki manukato, yapenyayo mtimani,
Kukuacha ni majuto, nitaingia tabani,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Tuwapo nawe pamoja, najihisi furahani,
Nasahau ni mseja, ahali sijapatani,
Huwa siioni haja, nikaha kutimizani,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Haja gani kumiliki, shamba madalibasari,
Wanyama na pikipiki, majumba nayo magari,
Ukakosa urafiki, ulo dhahiri shahiri,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Ulonionesha Mali, nikiwa nusu kaputi,
Ninajuwa ni halali, wangataka hawapati,
Wala sitowakubali, waichukue katiti,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Zaidi yako rafiki, sijapata kuwaona,
Wenzi wao manafiki, wasojua kupendana,
Siri zako hawaweki, wanasambaza bayana,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Wanahubiri u mui, hawakujui nasema,
Wakizua usodai, waniondoa naima,
Sasa sitopata bui, zaidi yakwe daima,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga naondoka.

Kaditama ewe mbasi, nalia nikiondoka,
Ujue yako nafasi, kamwe haitobanduka,
Ikiisha yangu kesi, mwenyewe nitakusaka,
Rafiki chupa ya bia, nakuaga nikiondoka

© Moses Chesire