Nakuasa Mwanangu

Songea karibu mwanangu, unisikize abuyo,
Kilete kigoda changu, pamoja na maswaliyo,
Ina mambo ulimwengu, uyadhaniayo siyo,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Kwanza chunguza rafiki, utembeao pamoja,
Wengine ni manafiki, wasokupea natija,
Watakungiza dhiki, kishe wapige pambaja,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Pili omba musamaha, mwenzako ukikosea,
Huzua tele furaha, muamana kuibua,
Mitima nayo huhaha, mizigoyo ukitua,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Mwanangu kunazo ndwele, zimengia kotekote,
Nyingine lau mshale, hufuma mwilini kote,
Hukuwachia mapele, yasopona kivyovyote,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Ndugu wa toka nitoke, waje kabula wengine,
Hili muhimu lishike, kuliko yale mengine,
Hawatakuacha peke, shida tabu zikufike,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Tena kuipiga dua, ndilo jambo la sharuti,
Ongeya naye jalia, japo iwe kwa katiti,
Atayafanya halua, maisha kisangalati,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Yasome vyote vitabu, usisaze nakujuza,
Ilimu huondoa tabu, na akili kukujaza,
Yote masitaajabu, tajua Pasi kusaza,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Heshima sikia kijana, haina gharama baba,
Waheshimu sanasana, wakaribu mahabuba,
Hiyo hukinga laana, nayo mibaya misiba,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani.

Baba yako nimechoka, naomba kutamatisha,
Hakika nilikofika, jamani kumenitosha,
Ukizishika hakika, maisha ‘tanawirisha,
Chukua yangu wasia, ifumbate kiganjani..

© Moses Chesire (Sumu la waridi)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *