Jembe Halilimi

Jembe langu nawajuza, limekuwa kiserema,
Halilimi linacheza, mchanga linaitema,
Sina budi kuliuza, na kwa Fundi kulisema,
Hili jembe kisirani, limedinda halilimi.

Zamani lilitifua, mashamba ya kila nui,
Katu halikuchagua, dongo lote liliwai,
Leo nakosa afua, jembe limeshuka bei,
Hili jembe kisirani, limedinda halilimi.

Nadhania lina kutu, limezuia kulima,
Au piya kuna kitu, kifanyacho kutetema,
Lanifanya sithubutu, kadamnasi kusema,
Hili jembe kisirani, limedinda halilimi.

Sina raha naungulika, limenitia tabani,
Ninajihisi hakika, nasengenywa mitaani,
Nikabadili silika, nagombani hadharani,
Hili jembe kisirani, limedinda halilimi.

Ndugu nitakuwa chizi, nyumbani nitamakani,
Niendee waganguzi, waniauni jamani,
Ninakosa usingizi, nimeingia mashakani,
Hili jembe kisirani, limedinda halilimi.

© Moses Chesire (Sumu la waridi)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *