Ulinizalia Nini?

Swali ninakusaili, wewe uliyenizaa,
Mbona usinikubali, mwanao nimeduwaa,
Ulofanya ukatili, hata nzi wamezubaa,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Starehe za mahaba, kasahau u mdogo,
Wavuli hadi wababa, kawapa penzi kidogo,
Wengine wakakukaba, ukawa kama kigogo,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Sasa ninatapatapa, kana kwamba ni yatima,
Sili kipande cha papa, kwa sababu yako mama,
Mlo naula kwa pupa, nisije pata dhuluma,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Shati langu ndilo mto, vibarazani nalala,
Natafuta hata moto, baridi isije nila,
Kelele za watoto, polisi na zao ala,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Nishapatwa na maradhi, kohozi hadi upele,
Mara ni barabarani, sina nyuma wala mbele,
Naitwa hayawani, kwani shida zangu tele,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Rabuka akusamehe, mamangu umenitosa,
Nalia sina sherehe, silijui langu kosa,
Wakati sija balehe, tena watu waniposa,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

Tamati nimefikia, nisije nikakufuru,
Kilio umesikia, hata uwe Buruburu,
Nakushukuru Jalia, nimewashibda kunguru,
Ulinizalia nini, iwapo hungenilea?

© Emmanuel Charo (Malenga Daktari)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *