Twataka Utunzi Bora

Mpangilio wa vina, tena kamili mizani,
Ukipanga vema dhana, ufasaha kwa makini,
Bila sana kujivuna, ila unajiamini,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Ulio bora uketo, tena ulio nasaha,
Ni kwa lugha ya mkato, isokosa ufasaha,
Aali ja manukato, pasipokuwa karaha,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Uzielewe arudhi, kusoma na kubukua,
Uzingatie mahadhi, shairi liwe murua,
Msiwanie ya hadhi, muhimu fani kukua,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Ifikapo ni kulumba, lunga pasi masihara,
Ulijue la kuamba, lako lije tia fora,
Likolee la kufumba, kwa za ushairi sera,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Tafiti vema huluka, mwanadamu kuelewa,
Uwapo ukiandika, tungo zikafurahiwa,
Tungo za kueleweka, na bora za kughaniwa,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Si maneno kutundika, wala iwe kushindana,
Haiwi kutambulika, ati kwa swifa kufana,
Bingwa si kufahamika, lakini ni kufaana,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

Tunga usipate fedha, uikuze hino fani,
Uketo wa mawaidha, tena wingi wa maoni,
Utunge kadha wa kadha, tungo bila walakini,
Twataka utunzi bora, ila si bora utunzi.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *