Mapinduzi Gerezani

Viumbe wenye uhai, Hapa sisi tumejaza,
Kujazana hatukai, Gereza limetumeza,
Wachache kutoa chai, Pazuri basi gereza,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Viumbe wakosa huru, Gereza limetufunga,
Jamii kutotuzuru, Hatujui sisi anga,
Wasiotoa ushuru, Ni sisi tusio mwanga,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Gerezani tulingiya, Wachochole hohehahe,
Twatoshana asiliya, Na basi twataka shehe,
Bila shaka ni raiya, Twataka akuwe shehe,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Na basi tunayo haki, Kiongozi kuchagua,
Kwa mabaya hausiki, Shida zetu kutatua,
Kwetu aziwe kiziki, Ndoto zetu kuziua,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Basi shehe kajuana, Na wakubwa wenye haki,
Kasahau sisi sana, Na tena haongeleki,
Kiburi tunachoona, Amepaa na hashuki,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Uhalisi wa gereza, Bayana wajitokeza,
shehe sasa hatuuza, Na sisi basi kuoza,
Nyoyoni tunayawaza, Wafungwa anatupwaza,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Nyoyoni tunajutiya, Mjukuu ‘ya majuto,
Mateso tunapitiya, Yanachoma kama moto,
Kwa wakubwa akoleya, Shehe wetu kwa mvuto,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Apendue shehe nani, Tuamini uyo nani,
Mchochole tuamini, Wasaliti hashikani,
Atupe matumaini, Ya kutoka gerezani,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Wa kusahau asiwe, Ni nyuma alikotoka,
Na wachochole wengine, Pasi kusahaulika,
Akule na sisi tuwe, Wa tumaini akika,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

Ukombozi gerezani, Mateso yatukaliya,
Wengi wapo kitanzini, Maisha ngumu waliya,
Basi waja kwaherini, Gerezani twaliliya,
Mapinduzi gerezani, Mpinduzi ndiye nani?

© Robinson Obaigwa

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *